Shindano la Ubunifu wa Mifumo ya Tehama (Hackathon)

Shindano la Ubunifu wa Mifumo ya Tehama (Hackathon)

Matumizi ya Tehama katika kutatua baadhi ya changamoto za Jiji la Mwanza

Katika juhudi zake za kukuza ubunifu na kukabiliana na changamoto mbali mbali nchini, Tume ya Taifa ya Sayansi (COSTECH) kwa kushirikiana na Atamizi yake ya DTBi, imeandaa mpango wa kuibua vipaji vya ubunifu katika Tehama kwa kutumia vijana wabunifu kutoka mkoani Mwanza kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Jiji la Mwanza.  Mpango huu unalenga kuwashindanisha wabunifu ambao watatakiwa kubuni mifumo ya Tehama itakayotatua changamoto kadhaa ambazo zimeibuliwa katika Warsha za wadau zilizofanyika Jijini Mwanza Tarehe 16/3/2017 na 18/3/2017 ambazo zimewahusisha wakuu wa idara za serikali Jijini Mwanza na wawakilishi wa wafanyibiashara katika Jiji la Mwanza. Washindi watapewa mafunzo na miongozo toka DTBi ili waweze kukamilisha ubunifu wao na kuweza kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine.

Changamoto No.1: Migogoro ya Ardhi

Migogoro ya ardhi imekuwa ni tatizo katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Mwanza. Migogoro hii imekuwa inasababishwa na matatizo ya mipaka, maingiliano kati ya wafugaji na wakulima na uelewa mdogo wa sheria za ardhi. Migogoro hii imekuwa kiini kikubwa cha ukosefu wa amani katika jamii na hata mara nyingine kusababisha mauaji kwenye jamii. 

Lengo

Kuwa na mfumo wa Tehama wenye ubunifu unaoweza kutoa ufumbuzi wa tatizo hili kwa kushirikisha jamii na serikali.

Matokeo

Kupata suluhisho la migogoro ya ardhi kwa kutumia ubunifu katika Tehama.

Changamoto No. 2: Usalama

Kumekuwa na tatizo kubwa la uvuvi haramu ndani ya ziwa Victoria unahatarisha mazalia ya samaki, takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2006 samaki waliovuliwa ziwa Victoria ni tani 676,000 wakati mwaka 2009 zilishuka hadi tani 331,000 (Hotuba ya Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda Dec 2009). Pili uhalifu huu huandamana na swala la usalama wa vyombo vya usafiri ndani ya ziwa kwani mara kwa mara wavuvi wamekuwa wanaibiwa injini za vyombo vyao na kunyanganywa samaki.

Lengo

Kuwa na mfumo utakaosaidia vyombo vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na matukio ya uvuvi haramu na uharamia ndani ya ziwa.

Matokeo

Kupunguza  na kudhibiti uvuvi haramu na uharamia ziwani

Changamoto no. 3: Utunzaji Kumbukumbu

Gharama ya utunzaji wa majalada ya kawaida ya Serikali imekua kubwa kwa maana ya uhifadhi, muda, upotevu na uhalifu, pamoja na gharama kubwa katika matumizi ya karatasi.

Lengo

Kuandaa mfumo wa Tehama utakaoweza kuhifadhi na kufuatilia majalada ya ofisi yanapopitia mikono mbali mbali ya watumishi na kuweka kumbukumbu sahihi.

Matokeo

Udhibiti madhubuti wa nyaraka za umma ili kuodoa usumbufu kwa wananchi.

Changamoto No.4: Msongamano Barabarani

Jiji la Mwanza ni kati ya majiji yanayokua haraka nchini Tanzania. Msongamano wa watu uliongezeka kutoka watu 945 mwaka 2002  hadi 1,420 mwaka 2012. Hali hii imeongeza tatizo la usafiri mkoani Mwanza linalosababishwa na msongamano wa magari barabarani. 

Lengo

Kuandaa mfumo wa Tehama utakaowezesha madereva kupata taarifa ya hali ya msongamano barabarani ili kufanya maamuzi sahihi kuhusu uchaguzi wa barabara ya kutumia isiyokuwa na msongamano.

Matokeo

Kupunguza muda wa kukaa barabarani kutokana na msongamano wa magari barabarani

Changamoto No.5: Elimu ya ujasiriamali

Jiji la Mwanza lina fursa nyingi katika maeneo ya ufugaji samaki, kuku na kilimo cha mboga na matunda. Ubora wa mazao kwa wazalishaji bado uko chini jambo linalowafanya wazalishaji kutokupata masoko ya uhakika yanayowawezesha kukuza kipato chao.

Lengo

Kuandaa mfumo wa Tehama utaowezesha wajasiriamali katika maeneo mbali mbali kupata elimu na majibu ya changamoto mbalimbali zinawakabili has katika ufugaji wa samaki, kilimo cha mboga na matunda na ufugaji wa kuku wa kisasa na kienyenyeji.

Mtokeo

Elimu ya ujasiriamali katika ufugaji kuku na samaki pamoja na kilimo cha mboga na matunda kuwafikia wafugani kwa urahisi na kipato kuongezeka

Changamoto No.6: Upashanaji Habari

Mawasiliano kati ya serikali za mitaa na wananchi ni jambo muhimu sana katika maendeleo ya jamii yoyote. Ni muhimu serikali kuwa na njia rahisi ya kuwafikishia wananchi wake habari kwa haraka hasa kunapokua na magonjwa ya milipuko, majanga ya mvua, matetemeko ya ardhi na kadhalika. Hivyo hivyo ni wajibu wa jamii kuwa na njia rahisi ya kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali na watumishi wengine wa serikali mara wanapokua na jambo linalohitaji hatua za haraka kutoka serikalini. Hii itaongeza uwajibikaji na kuchochea maendeleo katika jamii.

Lengo

Kuwa na mfumo wa Tehama utakaowezesha mawasiliano kwa urahisi kati ya viongozi wa serikali na wanachi wake au usambazaji wa taarifa muhimu toka serikali kwenda kwa wanachi kama vile bajeti na mipango ya halmashauri na utekelezaji wake. Pia kupata taarifa kutoka kwa wananchi kwenda kwa viongozi wa Serikali kwa wakati na kwa haraka.

Matokeo

Kuongezeka uwajibikaji wa watumishi wa umma kwa wananchi na kuondoa manunguniko kutoka kwenye jamii pamoja na kuiwezesha serikali kutoa huduma nzuri zaidi.

Mchakato wa kupata washindi

Tume ya sayansi (COSTECH) kwa kupitia Atamizi yake ya DTBi imeandaa shindano kwa wabunifu wa Tehama kutoka Mkoa wa Mwanza litakalofanyika tarehe 16/6/2017. Shindano hili litatanguliwa na mchakato wa wabunifu kufanya  maandalizi kwa njia ya “hackathon” kwa siku mbili kuanzia tarehe 14/6/2017 hadi 15/6/2017. Washindi wa shindano hili watawekwa chini ya Atamizi (DTBi) na kupewa huduma ya mafunzo, ushauri na miongozo hadi watakapokamilisha ubunifu wao na kuandaa mpango wa biashara ili kuwanufaisha wabunifu hao na jamii kwa ujumla.

Wabunifu wote wanaopenda kushiriki kwenye shindano hili wanatakiwa kutuma maombi kabla ya tarehe 31/5/2013 wakionyesha ni changamoto gani wanayotaka kuitatua, njia watakazotumia na timu itakayohusika kupitia  barua pepe ifuatayo; info@teknohama.or.tz  na kwa maelezo zaidi piga simu namba 0767452372 pia kwenye tovuti ya DTBi  www.teknohama.or.tz   au ya Tume www.costech.or.tz.

Wote watakaokubaliwa kushiriki kwenye shindano wataalikwa kwenye kikao maalum kitakachotoa ufafanuzi kuhusu  namna shindano na hackathon vitakavyoendeshwa 12/06/2017.

Vigezo va Kushiriki

Mshiriki awe mkazi na mbunifu anayeishi Jiji la Mwanza na awe raia wa Tanzania.

Awe na ujuzi wa kutosha katika kutengeneza program za Tehama au awe na mshirika mwenye uwezo huo.

Tuungane pamoja, hii ni fursa muhimu kwako na kwa maendeleo ya Mwanza